Wednesday, December 17, 2014

On 8:29 AM by Unknown   No comments


Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
SIKU yoyote wiki hii, Rais Jakaya Mrisho Kikwete atakata mzizi wa fitina juu ya sakata la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow. Macho na masikio ya kila mtanzania yameelekezwa kwake kwa matumaini kwamba hatua stahiki zitachukuliwa katika kutekeleza maazimio ya Bunge.
Watu wanategemea vigogo wote waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo watatendewa haki kwa kila mmoja kuhukumiwa kwa kadiri ya ushiriki wake katika ukwapuaji wa bilioni hizo 306, ambazo kimsingi ni nyingi sana.
Ninajua mbinu chafu zinazofanywa na baadhi ya waliohusika na wizi huu, kwa kuwatumia watu wa kada mbalimbali ili kuuaminisha umma kuwa fedha zilizochotwa, siyo za serikali, isipokuwa ni za IPTL. Tuliofuatilia sakata hilo tokea mwanzo, hatuna shaka ya uwepo wa fedha za wananchi ndani yake.
Lakini wakati tukisubiri kuona nini kitawapata Profesa Sospeter Muhongo, Profesa Anna Tibaijuka, Eliakim Maswi, Jaji Frederick Werema na Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, tunadhani ni wakati muafaka pia kwa Rais kutueleza kuhusu watu kutoka Ikulu waliotajwa katika ripoti ya PAC kuwa walishinikiza kutolewa kwa fedha hizo.
Tunahitaji ufafanuzi kutoka kwa Rais maana limeshakuwa jambo la kawaida sasa ofisi hiyo kubwa ya umma kutajwatajwa katika uchafu unaofanywa mitaani, kitu ambacho kisipodhibitiwa mapema, kinaweza kuharibu sifa yake kama taasisi.
Mtu mmoja anayeitwa Prosper Mbena, ambaye haijafahamika hasa kwa wadhifa upi alionao aliweza kutoa shinikizo hilo, si mtu wa kubeza. Ofisa wa Ikulu anapotajwa katika kashfa kama hii, ni vigumu wananchi kushindwa kuamini kuwa mkuu wa nchi alijua nini kinachoendelea.
Hatutaki kuamini kuwa serikali yetu, hasa Rais Kikwete alijua hujuma hii na akainyamazia. Kama hakujua, basi ni wakati muafaka kutueleza hatua zinazochukuliwa dhidi ya watu hawa.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Ikulu kutajwa katika mambo yanayoivunjia heshima wakati ni taasisi inayopaswa kuheshimika. Wakati ule wa sakata la utekwaji na uteswaji wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, ofisa mmoja wa ofisi hii alitajwa kuhusika katika mpango mzima wa tukio lile la kiharamia.
Serikali haikutoa majibu yaliyokidhi katika tuhuma hizi na hadi leo watu wanaamini kuhusika kwa ofisa huyo. Upo uwezekano mkubwa kwamba Rais Kikwete hafahamu lolote juu ya mambo ambayo ofisi yake inatajwa kuyajua. Maofisa wanatumia nyadhifa zao pale kufanya mambo ambayo yanaichafua Ikulu yetu.
Kama jambo hili linafanyika, basi ni lazima tukiri kuwepo kwa udhaifu mkubwa wa kiutendaji, ambao haupaswi kufumbiwa macho, kwa sababu ipo siku atauliwa mtu na Ikulu yetu itatajwa.
Tutakuwa nchi ya ajabu kama tutaruhusu sehemu ambayo muasisi wa taifa hili, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alipaita ni mahali patakatifu, leo pawe panatajwa kwa mambo mabaya, ya jinai na wizi. Tusiwaache maofisa wachache walioaminiwa, watumie jina lake ili kufanikisha malengo yao hasi.
Nikiamini kuwa Ikulu haitakubali kuendelea kuchafuliwa na maofisa wake, nirudie tena kumkumbusha Rais Kikwete kuwa wananchi wake wana matumaini makubwa sana ya kusikia akitoa kauli yenye kuonyesha kukerwa kwake na kilichotokea, kwa sababu mara zote amekuwa akijinasibu kama mlinzi namba moja wa rasilimali za taifa.
Nimalizie uchochezi wangu kwa kumuomba Rais Kikwete kucheza karata vizuri kwenye suala hili kwa sababu wizi huu umewachefua wengi na kama atachukua maamuzi yatakayowakingia kifua wahusika, linaweza kujikuta linakigharimu chama tawala katika uchaguzi mkuu ujao.

0 comments:

Post a Comment