Thursday, December 25, 2014

On 10:38 PM by Unknown   No comments
MWAKA 2014 unatarajiwa kufikia mwisho wake Jumatano ijayo saa sita kamili usiku. Ni mwisho wa siku 365 ambazo Watanzania, kama walivyo watu wengine kote duniani, watakuwa wakiutumia pia kuomboleza vifo vya wasanii wao wa fani mbalimbali, hasa muziki na filamu, ambao walifariki kwa karibu miaka mitatu iliyopita.
Tunapozungumzia kifo, wote tunajua kuwa ni fumbo ambalo daima ni Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa kulifumbua. Kila nafsi iliyo hai itaonja mauti, ingawa kinachotofautisha kati yangu na yako, ni kwamba hakuna ajuaye siku wala saa.
Mtu mwenye afya kamili kabisa anaweza kudondoka sasa hivi na kuwa marehemu, wakati mwingine aliyekata kauli zaidi ya miaka mitatu iliyopita akiwa bado anapumua kitandani. Hapa ndipo tunapokutana na umwamba wa Mungu Mwenyezi, Muumba wa Mbingu na Ardhi.
Hata hivyo, pamoja na uwezo wa Mungu katika kuamua kuhusu uhai wetu, bado sisi wenyewe kama binadamu, tunao uwezo wa kutengeneza mazingira ya kulazimisha kukatishwa kwa maisha yetu, kutokana na staili ya maisha tuliyoamua kuifuata.
Baadhi tumeamua kuwa walevi wa kupindukia. Ni dhahiri, ukiwa mlevi wa namna hii, kifo chako kinakuwa jirani zaidi kwa sababu katika akili za kilevi, huna uwezo wa kuchukua tahadhari wakati wa kuvuka barabara, huna uchaguzi wa maneno ya kuongea kiasi cha kumkasirisha mwenzako na pia akili ndogo za kutambua kuwa wingi huu wa maji ya mvua katika mto unaweza kukusomba na kufa maji.
Wakati tukimaliza mwaka na kuwaombea Mungu awape mapumziko mema huko walikolala wasanii wetu waliofariki, yapo maneno kwamba baadhi yao walipoteza maisha kutokana na kujihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya, kitu ambacho kimetajwa kuwa ni hatari zaidi kwa wasanii wetu kutokana na aina yao ya maisha.
Ingawa haijathibitishwa, lakini vifo vya wasanii kama Langa Kileo, Albert Mangweha ‘Ngwea’, Aisha Madinda, Geez Mabovu na YP vinahusishwa na utumiaji wa madawa ya kulevya. Ni vigumu, kama nilivyosema mwanzo, kuthibitisha kuwa walifariki kwa sababu hiyo, lakini angalau ushahidi wa mazingira unaonyesha kuwa walikuwa ‘wananusa.’
Na hata hivi tunavyozungumza, ipo orodha ndefu ya wasanii wanaotajwa kujihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya, licha ya kila mmoja kwa wakati wake, wanakataa kutumia, ingawa sura za ‘mateja’ hazijifichi.
Historia inaonyesha kuwa mastaa wengi maarufu wa nje waliowahi kuripotiwa kutumia kilevi hiki, ama walifilisika, au walifariki vifo vya ajabu na ghafla. Mkali wa kufokafoka miaka ya 1990, Shabba Ranks alitoweka katika ramani ya muziki baada ya kuendekeza unga, kabla ya mbwiaji mwingine, Britney Huston kufariki baada ya kuzidiwa na dozi.
Hapa nyumbani, wasanii kadhaa wanatajwa kutumia madawa ya kulevya, kitu kinachohatarisha ustawi wao kisanaa na hata kiuchumi. Hakuna ubishi kuwa ‘unga’ umepunguza, kama siyo kusimamisha kabisa kasi ya Ray C kimuziki. Baada ya kukataa mara kadhaa, hatimaye ilithibitika kuwa ni ‘teja’ kiasi cha kumlazimu Rais Kikwete kuingiza nguvu zake kumuokoa.
Nyota wa muziki wa dansi, Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ ni msanii mwingine mwenye uwezo mkubwa kisanaa lakini anaogelea katika umasikini kutokana na kuendekeza matumizi ya unga, kama ilivyo pia kwa Msafiri Said maarufu kama Diouf.
Kama siyo matumizi ya madawa ya kulevya, huenda hivi sasa Rashid Makwiro ‘Chiz Benz’ angekuwa hakamatiki katika Bongo Fleva, lakini unga umemfanya siyo tu kupoteza uwezo wake wa kazi, bali hata muonekano wa mwili wake uliokuwa mkakamavu, hivi sasa anaonekana kama mtu anayeumwa.
Orodha yao ni ndefu, lakini itoshe kuwataja mastaa wanaosikitisha, ambao vipaji vyao vikubwa vinamalizwa na madawa ya kulevya kuwa ni pamoja na Q Chillar, TID, Blu, Greyson Semsekwa na muimba Injili nyota, Rose Muhando.
Madawa pia yanamaliza enzi za 20 Percent, Da Hustle, Daz Baba na Lord Eyez.
Licha ya hao, pia idadi ya wasanii wachanga na wenye majina wanaotajwa kujihusisha na ubugiaji huo wa sembe ni kubwa. Inadaiwa pia kuwa mwanzo wa wasanii wetu kutumia unga, unatokana na ukweli kwamba asilimia kubwa kati yao, ni wavutaji wa bangi.
Wakati fulani Ray C, akielezea ushuhuda wake wa jinsi alivyoanza kujiingiza katika ulevi huo, alisema awali hakujua kama alikuwa anavuta unga, kwani aliyekuwa mpenzi wake wakati huo, Lord Eyez alikuwa akimchanganyia kwenye bangi bila yeye kujua.
Kama msanii huyu ambaye sura yake iliashiria binti mrembo asiyetarajiwa kuwa na tabia ya uvutaji bangi, aliweza kupuliza, ni wazi kuwa asilimia kubwa ya wasanii hasa wa Bongo Fleva ni wavuta bangi.
Ni vigumu kuwaokoa waliokwisha zama katika shimo hili la uteja, lakini nafasi bado ni kubwa kwa wasanii wakubwa na wanaoheshimika kufanya juhudi za makusudi kutoa elimu kwa wasanii wachanga ili kuwafanya kutambua ubaya wa tabia hii.
Ni wazi kwamba wasanii kama Profesa Jay, Ambwene Yessaya, Mwana FA, Fid Q, Lady Jaydee na wakongwe wengine, wanaweza kuendesha kampeni za kuwaasa vijana kuachana na ulimbukeni huo, kwa sababu angalau wao, wameendelea kubakia katika levo za juu, licha ya kuwa katika gemu kwa muda mrefu huku kashfa kama hizi zikiwapitia kando.

0 comments:

Post a Comment